Toleo Jipya
Toleo Wiki Jana
Tuwasiliane
  

Wazanzibari tumieni busara sio nguvu kuiokoa nchi

Toleo Na. 098

Tahariri
KATIKA safu hii wiki iliyopita, tulitaka vyama vya CCM na CUF virudi mezani ili kukamilisha mchakato wa utekelezaji wa muafaka uliofikiwa baada ya miezi 14 ya majadiliano...
Na Saed Kubenea
“HUU si ushindi wangu binafsi, bali ni ushindi wa Watanzania. Ni ushindi wa wazalendo wa nchi hii, dhidi ya mafisadi. Hakika, huu ni ushindi wa wananchi wazalendo wa kweli katika taifa lao"...
Na Jabir Idrissa
ZIPO fitna tatu kuu kwa sasa zinazohusiana na hali ya mambo ilivyo Zanzibar kisiasa kiasi cha kukumbusha mabaya yaliyotokea mara tu baada ya uvurugaji matokeo ya uchaguzi mkuu wa 1995 na 2000...
Na Stanislaus Kirobo
Tangu ateuliwe kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu takriban miezi mitatu iluiyopita, Mizengo Pinda amemwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika shughuli za nje ya nchi mara tatu. Kwa wastani amefanya hivyo mara moja kila mwezi...
Na Joseph Mihangwa
HAKIKA, Zanzibar inaumwa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kama kuna maneno sahihi ya kuelezea kiwango cha ugonjwa wake, ni kwamba “Zanzibar sasa imo katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU)...
Na Mbasha Asenga
KUNA uvumi uliotamalaki kwamba ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), lipo kundi la watu linalojiandaa kumpinga rais wao mwaka 2010....
Na Saed Kubenea
KATIKA siku za karibuni, mmoja wa wanasiasa wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Job Lusinde, ametoa kauli kwamba watuhumiwa wa ufisadi wenye nyadhifa ndani ya chama hicho wavuliwe uwanachama...
Na Mwandishi Wetu
KAMA kuna jambo ambalo baadhi ya Watanzania wenzetu hawajafuzu, ni mwenendo wa siasa za ushindani zinazohusisha chama tawala na vyama vya upinzani...
Na Fareed Zakaria
Mwezi uliopita kura moja mpya ya maoni ilionyesha kwamba asilimia 81 ya Wamarekani wanaamini kwamba nchi yao iko katika mwelekeo usio sahihi...
Na Bakari Makusudi
KUONDOKA nchini Tanzania kwa uongozi wa juu wa kikundi pekee cha waasi kinachoendeleza vita dhidi ya serikali ya Burundi inayoongozwa na kilichokuwa kikundi cha waasi cha CNDD-FDD kunafungua ukurasa mpya kisiasa nchini Burundi....
Na Joseph Mihangwa

HAKIKA, Zanzibar inaumwa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kama kuna maneno sahihi ya kuelezea kiwango cha ugonjwa wake, ni kwamba “Zanzibar sasa imo katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Ule mpasuko wa kisiasa uliokuwapo miaka ya nyuma, sasa umezidi kushika kasi kiasi cha kutishia umoja wa kitaifa na hata umwagaji damu.

Mpasuko huu unaiondolea nchi hii sifa ya kale kama kitovu cha ustaarabu, dini, biashara, historia na mambo mengine. Ni dhahiri ugonjwa huu, umeifanya Zanzibar kuwa goigoi; taifa limekuwa la kuangalia nyuma badala ya kwenda mbele.

Fitina na chuki kwa misingi ya historia na ubaguzi wa rangi zimepandwa na kumea ndani ya jamii ya Kizanzibari na kuzaa uhasama wa kutisha unaotishia kuangamiza taifa.

Kila kukicha tunawasikia viongozi wa kisiasa wakisema, “Tunanoa mapanga yetu (ya mapinduzi) ya 1964”. Mara moja mtu makini anajiuliza, nani tena anataka kupinduliwa?

Wengine utawasikia, “tutalinda Muungano kwa nguvu zote?” sijui nani mwenye hati miliki ya kutawala Zanzibar mbali na Wazanzibari wenyewe?

Au nani anasema muungano ni hoja; au ni Mtanzania gani asiyeutaka Muungano? Ya nini kulia “Mbweha” pasipo Mbweha? Huu ni woga, au unafiki?

Kila panapochomoza mwanga wa jua huashiria kumekucha. Ili Wazanzibari waamke, wanasiasa ni mafundi wa kutunga maneno na vibwagizo. Ni hao wanaonufaika na hali ya giza; Zanzibar inasumbuliwa na mzimu wa  watu wa kale.

Wapo wanaotukuza historia iliyojaa vituko na umwagaji damu; wenye kutukuza tofauti za kitabaka, kwamba wale wanaoishi leo au ndugu zao hawastahilil kuurithi “ufalme.”

Kwao, suluhisho pekee la kutatua migogoro ni kuwajaza wananchi fikra kwamba hakuna mwingine mwenye haki ya kuongoza Zanzibar, zaidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwamba, ile ahadi ya Hayati Abeid Amani Karume ya kufanyika uchaguzi huru na haki Zanzibar baada ya miaka 50 (tangu mapinduzi 1964) haijatimia.

Wapo pia baadhi ya Wazanzibari wanaoona kwamba mpasuko wa kisiasa Zanzibar una mizizi ya kihistoria kuanzia na maasi/ya machafuko ya mwaka 1936, 1957, 1961 na Mapinduzi ya 1964. Hawa wanaona kuwa huo ni utamaduni wa Kizanzibari wa umwagaji damu usiofutika.

Lakini tujiulize: Historia ilikwenda wapi kati ya miaka ya 1970 na 1980 ambapo, Tanzania, chini ya uongozi shupavu wa Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zilishuhudia hali ya upendo, amani na utulivu?

Je, hili sokomoko la sasa linaanzia wapi? Mimi naamini kwamba Wazanzibari hawakugawanyika kitabaka, kimajimbo au kirangi, ila kuna juhudi za walafi wachache kutaka kuwagawa kwa manufaa ya kisiasa.

Wapo wanaoamini kuwa matatizo ya Zanzibar yanasababishwa na Serikali ya Muungano yenye kumiliki Jeshi, Polisi na vyombo vingine vya ulinzi. Kwamba Zanzibar inakandamizwa na Muungano; matatizo yake si ya Tanzania kama nchi.

Pengine ni kwa sababu hii, ndiyo maana Rais Amani Abeid Karume alipata ujasiri wa kuwambia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake huko Butiama kwamba “vikao vya CCM haviwezi kuwaamulia Wazanzibari jinsi ya kutawala nchi yao.”

 na baadhi ya wajumbe  hawa wanaamini kwamba muundo wa Muungano una matatizo yanayozaa machafuko yasiyo na ufumbuzi. Na kila “vurugu”zinapotokea wao huandaa “muafaka”kujaribu kutibu dalili za ugonjwa badala ya kutibu ugonjwa wenyewe.

Historia imeonyesha hata hivyo kwamba kile kinachoitwa “juhudi za kufikia Muafaka”huwa ni hadaa tu kutafuta amani na utulivu wa muda. Mara zote utawala madarakani hua hauoko wazi, na mara nyingi hubeba ajenda ya  siri ya kubakia madarakani. Na mwisho wa yote huwa hapana “mwafaka” wowote.

Haya yalijidhihirisha kwa Muafaka wa kwanza (The Accra Accord) mwaka 1958 kati ya ZNP na ASP; na 2001 kati ya CCM na CUF Zanzibar, ambapo Tume ya pamoja ya Rais ilifanya kazi nzuri sana na kuleta mabadiliko muhimu, kama vile kuundwa upya kwa Tume ya Uchaguzi, kuanzishwa kwa daftari la kudumu la wapiga kura, na kwa CCM na CUF kurejesha mahusiano ambapo kwa mara ya kwanza vyama hivi  viliweza kukutana na kukubaliana namna ya kuendesha kampeni.

Kama tulivyosema, siasa za Zanzibar ni za ajabu sana. Mara Mzimu wa kale ukaibuka wakati za kampeni za 2005, na maneno ya uhasama na shari yakaanza kutamkwa kama (Karume):  “Lolote lisilotarajiwa (matokeo ya uchaguzi) likitokea, tuko tayari kutumia silaha za Mapinduzi ya 1964, kwani CCM Zanzibar wanazo funguo za sanduku la silaha   hizo”.

Au (Mapuri), “Uhuru wa Zanzibar ulipatikana kwa mapanga, hivyo hauwezi kukabidhiwa kwa yeyote kwa njia ya sanduku la kura”. 

Naye Rais Amani Abeid Karume, wakati akiapishwa mwaka 2005 baada ya kushinda uchaguzi alisema,”CCM Zanzibar haina historia, wala haiwezi kuwa na utamaduni wa kuunda serikali ya mseto”.

Wakati juhudi za sasa za “Muafaka”mpya zikiendelea Visiwani, Viongozi wake hawajakanusha, kuzifuta wala kuzikana kauli zao hizo  kuufanya umma uamini kwamba wanayo nia thabiti kwa juhudi zinazoendelea.  Bila kufanya hivyo tunashawishika kuamini kwamba juhudi hizi ni geresha tu na zitashindwa kama jinsi juhudi za nyuma zilivyoshindwa .

Kama hivi ndivyo, kwa nini tunapoteza fedha nyingi za umma kuusaka muafaka eti kwa njia ya mlango wazi, wakati mioyo yetu imefungwa?.  Tuiiteje tabia hii? Unafiki? Ubabaishaji? Usultani mpya?.

Tatizo kubwa lililopo ni mpasuko wa kisiasa kati ya Unguja ambayo imeshikwa na CCM, kuanzia madiwani hadi wawakilishi; na Pemba, ambayo imeshikwa na CUF kwa kiwango hicho hicho.  Hata kabla ya uhuru kundi moja la vyama vya siasa lilikuwa  na nguvu zaidi Unguja na udhaifu Pemba, na kundi la pili lilikuwa na nguvu zaidi Pemba na udhaifu Unguja.

 Ilivyo sasa, Wananchi wa Unguja wanaona wanayo serikali, na Wapemba wanaona wamekuwa pembeni.  Ni historia kujirudia, kwamba tangu utawala wa Mzee Abeid Karume, viongozi wa zamani wa vyama mbali na ASP walitumika kwa shughuli za kitaaluma tu, na ilikuwa marufuku kwao kupewa nafasi za uongozi wa kisiasa ndani ya Chama, Serikali ya Mapinduzi na katika Serikali Muungano.

Kuendekeza  hali hii kunaashiria kwamba, Zanzibar imefungua milango kwa mfumo wa vyama vingi bila kufungua moyo.  Wameukubali mfumo lakini hawataki kutekeleza matakwa ya demokrasia chini ya mfumo huo.  Huu ndio mwanzo wa tatizo ambalo pia litaendelea kuitikisa serikali ya Muungano.

Kwa hali ya sasa, na kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere mwaka 1995, “Kama si Muungano, Zanzibar haipo, kuna Unguja na Pemba.  Hivyo kwa kutambua hilo, kuna umuhimu kuchukua hatua ya kuziunganisha unguja na Pemba ili kuimarisha Muungano. Njia moja ya kufanya hivyo ni kwa serikali kuwa mikononi mwa CCM, lakini nafasi ya vyama vya upinzani itambuliwe kikamilifu katika uongozi wa nchi.

Tujifunze kutoka Msumbiji ambako   baada ya Mapambano ya silaha msituni  ya muda mrefu, kati ya vyama vya FRELIMO na RENAMO, walikaa na kuelewana kufuatia matokeo ya uchaguzi yanayofanana sana na haya  kati ya CCM na CUF Zanzibar,  wakakubaliana kushiriki kwenye Bunge kuunda serikali.  FRELIMO na RENAMO vinatambuana na kuheshimiana.

Nako huko Afrika Kusini, mwaka 1994, ANC ilishinda uchaguzi kwa kiwango kikubwa na ingeweza kuunda serikali bila kushirikisha vyama vingine.  Lakini kwa kuwa kulikuwa na mgawanyiko mkubwa, ANC iliona busara kushirikisha vyama vingi (hata vile vidogo) kuunda serikali ili kujenga umoja wa kitaifa. Bila kutaja mafanikio kama hayo nchini Kenya hivi karibuni, utaratibu huu ndio ulio muafaka katika mazingira ambapo vyama viwili vya siasa vinalingana nguvu.

Kama wapigania uhuru wa msituni huko Msumbiji na Afrika Kusini waliotumia  siraha kali na nzito na akili kuharibika wameweza kuungana, kwa nini “wanamapinduzi wa mapanga”tu Zanzibar washindwe kujenga taifa moja?.  Busara, badala ya nguvu na ujanja, itumike kuiokoa Zanzibar. Muafaka makini utakuwa ni kielelezo cha uwezo wa kutatua matatizo kwa manufaa yao.